Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amelitaka shirika la Bima la taifa (NIC) kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu ya Bima inamfikia kila mtu ili kufikia malengo ya serikali ifikapo 2030 asilimia 90 ya watanzania kuwa na uelewa kuhusu Bima lakini pia kuwa na Bima ya maisha.
Hayo ameyasema jijini Dar es salaam wakati akifungua semina ya siku moja ya mawakala wa bima iliyoandaliwa na NIC kwa kushirikiana na wakala wa Bima wa Taifa pamoja na TIRA.
Amesema NIC ina jukumu kubwa la kuhakikisha inahamasisha mawakala wa Bima kutoa elimu kwa jamii na kuhakisha watu wanajiunga katika Bima zao ili kusaidia uelewa mpana wa shughuli za Bima katika maisha ya kila siku.
“NIC naiagiza ikae na wadau wake mbalimbali wajadili ili kuhakikisha Bima inakuwa muhimu kwa kila mtanzania waifikirie kama anavyofikiria kula”amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa semina hiyo inatarajiwa kujadili mpango utakaowezesha kufikia 2030 kila mtanzania anakuwa na uelewa kuhusu Bima lakini pia kumiliki Bima.
Sambamba na hayo Chalamila amewataka TIRA kujikita kwenye kuwezesha mawakala na si kuishia kwenye udhibiti pekee.
Aidha Chalamila amewapongeza Mawakala wa Bima kwa kupiga hatua kwenye Bima ya Afya na kuwataka wajitahidi kuboresha kwenye Bima za magari.
“Mawakala mkae mjaribu kutathimi na kuweka mikakati ya namna ya kumsaidia mtu alielipa Bima kwa miaka mingi lakini ajawahi kupata na shida ambayo ingemtaka wakala wa Bima kumsaidia hii itasaidia kuongeza idadi ya watu wanaohitaji kujiunga na Bima zenu”amesema Chalamila.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Bima nchini(IAAT)Sayi Daud ameiomba serikali kuondoa tozo mbalimbali ambazo zimekua kikwazo kwa mawakala hao.
“Ombi letu kwako mkuu wa mkoa tunaomba uzungumze na halmashauri watuondolee kodi ya mabango lakini pia kodi ya huduma ambayo kimsingi ilitakiwa itolewe na makampuni”amesema Daud
Nae Meneja ukaguzi TIRA Frank Shangali amesema sekta ya Bima inatoa ajira zaidi ya 2000 zinazozalishwa kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni kila mwaka.
Hata hivyo mkurugenzi wa bima za maisha Hadbert Polepole ambaye amemuwakilisha Mtendaji Mkuu wa NIC amesema wamekua wakifanya kazi na mawakala kwa miaka 60 sasa na kazi hiyo imekua na tija kwa taifa.
Amesema shirika hilo limeweza kufikia jamii kupitia mawakala hao hivyo muunganiko wao umekua ni tija na fursa.
“NIC tunaendelea kufanya kazi na mawakala lakini pia kuongeza mawakala wapya ili kufikia malengo ya serikali kuhakikisha sekta ya Bima inakua”amesema Polepole.
Nae Meneja Biashara NIC Kafiti Kafiti amesema shirika hilo ndio shirika kiongozi katika mashirika ya Bima kwani lina zaidi ya mawakala 70 katika Bima za maisha na Bima za ajali na magari.